Deuteronomy 7:12-24

Baraka Za Utiifu

(Kumbukumbu 28:1-14)

12 aKama mkizingatia sheria hizi na kuzifuata kwa uangalifu, basi Bwana Mungu wenu atatunza Agano lake la upendo nanyi, kama alivyowaapia baba zenu. 13 bAtawapenda ninyi na kuwabariki na kuongeza idadi yenu. Atabariki uzao wa tumbo lenu, mazao ya nchi yenu, nafaka, divai mpya na mafuta, ndama za ngʼombe wa makundi yenu, na kondoo za makundi yenu katika nchi ile aliyoapa kuwapa baba zenu. 14 cMtabarikiwa kuliko mataifa mengine yote, hakuna wanaume wala wanawake kwenu watakaokosa watoto, wala mifugo yenu haitakuwa tasa. 15Bwana atawakinga na kila ugonjwa. Mungu hatatia juu yenu ugonjwa wowote mbaya mlioufahamu huko Misri, lakini atatia ugonjwa juu ya wale wote wanaokuchukia. 16 dNi lazima mwangamize watu wote ambao Bwana Mungu wenu atawatia mikononi mwenu. Msiwatazame kwa kuwahurumia na msiitumikie miungu yao, kwa kuwa itakuwa mtego kwenu.

17 eMnaweza kujiuliza wenyewe “Mataifa haya ni yenye nguvu kuliko sisi. Tutawezaje kuwafukuza?” 18 fLakini msiwaogope. Kumbukeni vyema jinsi Bwana Mungu wenu alivyofanya kwa Farao na kwa wote huko Misri. 19 gMliona kwa macho yenu wenyewe majaribu makubwa, ishara za miujiza na maajabu, mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, ambao kwa huo Bwana Mungu wenu aliwatoa mtoke Misri. Bwana Mungu wenu atawafanyia hivyo watu wote ambao mnawaogopa sasa. 20 hZaidi ya hayo, Bwana Mungu wenu atatuma manyigu miongoni mwao hadi yale mabaki watakaojificha waangamie. 21 iMsiingiwe na hofu kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu, ambaye yupo miongoni mwenu ni mkuu naye ni Mungu wa kutisha. 22 jBwana Mungu wenu atawafukuza mataifa hayo mbele yenu kidogo kidogo. Hamtaruhusiwa kuwaondoa wote kwa mara moja, la sivyo wanyama mwitu wataongezeka na kuwa karibu nanyi. 23 kLakini Bwana Mungu wenu atawatia watu hao mikononi mwenu, akiwatia katika kuchanganyikiwa kukubwa mpaka wawe wameangamizwa. 24 lAtawatia wafalme wao mikononi mwenu, nanyi mtayafuta majina yao chini ya mbingu. Hakuna hata mmoja atakayeweza kusimama dhidi yenu bali mtawaangamiza.
Copyright information for SwhNEN